
Baada ya taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mrema kuvuliwa uanachama CHADEMA na Tawi la Bonyokwa la chama hicho, Mrema ameibuka na kukanusha taarifa hiyo.
Akizungumza kupitia taarifa rasmi kwa vyombo vya habari, Mrema amesema barua hiyo haina uhalali wowote kwani haikubainisha namba yake ya uanachama, jambo ambalo ni kinyume na Kanuni za Chama kifungu cha 5.1 na 5.2 ambavyo hutambua wanachama kwa namba za kadi.
Amefafanua zaidi kuwa hajasajiliwa kwenye Tawi la Bonyokwa kama ilivyoelezwa, bali ni mwanachama wa Tawi la Makongo, na taarifa hizo zinapatikana kwenye mfumo rasmi wa kidijitali wa CHADEMA.
Aidha, amesema hajawahi kushiriki kikao chochote cha tawi la Bonyokwa na hivyo hatua ya tawi hilo kumvua uanachama haina msingi kisheria ndani ya chama.
Mrema amesema Kanuni ya 5.3 ya CHADEMA inaweka wazi utaratibu wa mwanachama kuhama kutoka tawi moja kwenda jingine, na yeye hajawahi kuwasilisha taarifa ya kujiunga na Bonyokwa. Kwa msingi huo, amesema hana uhusiano wowote na tawi hilo na halina mamlaka ya kuchukua hatua dhidi yake.
“Kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama, mimi bado ni mwanachama halali wa CHADEMA mpaka hapo hatua rasmi za kinidhamu zitakapochukuliwa dhidi yangu na mamlaka husika,” amesema Mrema.
Ameongeza kuwa ataendelea kutimiza wajibu wake kama mwanachama wa chama hicho kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama.