
Kufikia mwaka 2025, taswira ya mabilionea duniani inaongozwa na nchi chache zilizotawala kwa kiasi kikubwa, ambapo Marekani inaongoza kwa tofauti kubwa.
Takwimu za hivi karibuni kutoka kwenye orodha ya Forbes World’s Billionaires List, zinaonesha kuwa Marekani ina zaidi ya mabilionea 900, huku China, India na baadhi ya nchi za Ulaya zikifuata kwa idadi kubwa ya mabilionea pia.
Hata hivyo, utajiri huu mkubwa umejikita zaidi katika nchi chache, ambapo mataifa matatu tu, Marekani, China na India, yanachangia zaidi ya asilimia 50 ya jumla ya mabilionea na utajiri wao duniani. Kinyume chake, kuna mataifa 17 ambayo kila moja lina bilionea mmoja tu.
Marekani inaendelea kutawala orodha hiyo kwa kuwa na mabilionea 902 mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko kutoka 813 mwaka uliopita, na wanamiliki jumla ya utajiri wa dola trilioni 6.8 [TZS quadrilioni 18.3].
Hii ni orodha ya nchi kumi zilizo na idadi kubwa ya mabilionea mwaka 2025;
1. Marekani: 902
2. China: 450
3. India: 205
4. Ujerumani: 171
5. Urusi: 140
6. Canada: 76
7. Italia: 74
8. Hong Kong*: 66
9. Brazili: 56
10. Uingereza: 55
*Hong Kong si nchi huru, bali ni Eneo Maalum ya Utawala (SAR) chini ya Jamhuri ya Watu wa China. Hata hivyo, hutajwa pekee yake kutokana na mfumo wake wa kiuchumi na kisheria unaotofautiana na ule wa China.
Chanzo: Business Insider