Serikali kuanzisha leseni maalum ya uzalishaji chumvi

0
3

Serikali ipo mbioni kutambulisha leseni mpya ya uzalishaji wa chumvi ili kuiondoa chumvi katika kundi la madini mengine na hivyo kuchochea ukuaji wa tasnia ya uzalishaji chumvi nchini Tanzania.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dodoma wakati wa Kikao cha Waziri wa Madini, Anthony Mavunde na uongozi wa Chama cha Wazalisha Chumvi Tanzania (TASPA), kikao ambacho kimelenga kuboresha sekta ya madini kupitia tasnia ya chumvi.

“Serikali imesikia kilio chenu cha muda mrefu cha uwepo wa Leseni moja ya uzalishaji wa Chumvi ambayo itasaidia kumuendeleza mzalishaji chumvi kwa kupunguza gharama za uzalishaji na kuyaondoa madini chumvi katika kundi la madini mengine.

Naelekeza kuanza mara moja mchakato wa mabadiliko ya sheria ili kuruhusu uanzishwaji wa Leseni maalum ya uzalishaji chumvi ambayo pia tozo yake kwa hekta iangaliwe upya kufikia 20,000 kutoka kiwango kilichopo sasa,” amesema.

Amesema dhamira ya serikali ni kuona wazalishaji wa chumvi wanaongeza tija na kufikia hatua ya kumiliki viwanda vya uchakataji na usafishaji chumvi nchini ili chumvi yetu iwe yenye ubora na shindani.