Yanga yagoma kucheza Dabi, yasema mamlaka za soka chini zinatenda dhulma

0
4

Baada ya kesi Yanga SC kutupiliwa mbali na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS), Uongozi wa klabu hiyo umesema msimamo wao juu ya kutoshiriki mchezo namba 184 dhidi ya Simba SC wa Ligi Kuu msimu huu uko pale pale.

Barua iliyotolewa na CAS wiki iliyopita, iliielekeza klabu hiyo kurudi kwenye kamati za ndani za soka ili kushughulikia kesi yao kabla ya kurudi kwao kwa ajili ya hatua za rufaa.

Hata hivyo, Yanga SC imesema haina imani na haiko tayari kupeleka shauri hilo kwenye kamati za ndani za soka kama ilivyoelekeza CAS kutokana na uonevu, uvunjwaji mkubwa wa kanuni na upendeleo kwa baadhi ya timu unaoendelea kufanywa na mamlaka za soka nchini.

“Kutokana na uonevu, uvunjwaji mkubwa wa kanuni na upendeleo wa dhahiri kwa baadhi ya timu unaoendelea kufanywa na Mamlaka za soka Tanzania, uongozi wa Young Africans Sports Club hauna imani na hauko tayari kupeleka shauri hilo kwenye mamlaka ambazo zinatenda dhulma,” imesema taarifa ya Yanga SC.

Aidha, Yanga SC imesema Wanayanga wote watakuwa tayari kuipambania haki yao kivyovyote vile ili kukomesha dhulma na uvunjwaji mkubwa wa kikanuni unaoendelea kufanywa na mamlaka za soka kwa maslahi mapana ya maendeleo ya soka nchini.