
Ngao (Push bumper, bull bar, nudge bar, au brush guard kutegemea muundo na matumizi) ni kifaa cha chuma au plastiki kigumu kinachowekwa mbele ya gari, hasa magari ya polisi, SUV, au magari ya barabarani kwa sababu mbalimbali.
Ngao hizi ambazo mara nyingi hutengenezwa kwa chuma kigumu au plastiki ngumu, hufungwa mbele ya gari kwa lengo la kulinda sehemu ya mbele ya gari (radiator, grili, taa) dhidi ya uharibifu mdogo unaotokana na migongano midogo, kusukuma gari lingine linalokwama bila kuharibu gari linalosukuma na hata kupamba mwonekano wa gari.
Ngao za mbele za magari, maarufu kama push bumpers au bull bars, zimeendelea kutumiwa miongoni mwa madereva wa magari ya huduma, SUV na hata magari ya kawaida hapa nchini, huku wataalamu wa usalama barabarani wakionya kuhusu madhara yake.
Vyuma hivi, vilikuwa vinawekwa mbele ya magari hasa makubwa yanayopita kwenye maeneo yenye changamoto za wanyama wanaokatisha barabarani hasa ng’ombe au nyati. Vilevile magari yanayokwenda mbungani ili kuweza kuikinga gari na waliomo ndani dhidi ya madhara ya kugongana na wanyama.
Hata hivyo, wataalamu wa magari na usalama wa barabarani wanasema licha ya faida zake, ngao hizo zinaweza kuwa hatari kwa usalama wa watumiaji wengine wa barabara, hususan watembea kwa miguu na waendesha bodaboda.
Mbali na hayo, ngao hizo zinaweza kuathiri mfumo wa airbag wa gari, na kusababisha kushindwa kufunguka kwa wakati wa ajali. Pia baadhi ya magari ya kisasa yenye teknolojia ya kisasa kama sensor za kuepuka ajali au parking assist huathirika vibaya iwapo ngao hizo zimefungwa kiholela.
Baadhi ya nchi kama Australia na Uingereza zimeweka viwango maalum vya uzalishaji na matumizi yake ili kulinda watumiaji wengine wa barabara.