
Jeshi la Polisi mkoani Mara linamshikilia Macherege Wambura (52) mkazi wa Kijiji cha Robanda Wilaya ya Serengeti mkoani Mara kwa tuhuma za mauaji ya Jane Baragwa Nyamosenga (45) chanzo kikitajwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Kwa mujibu wa Polisi, tukio hilo limetokea Mei 21, 2025, majira ya asubuhi katika kijiji hicho, ambapo mtuhumiwa alimshambulia Jane kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali maeneo mbalimbali ya mwili wake na kusababisha kumwaga damu nyingi hali iliyopelekea kifo chake.
“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa, chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi ambapo mtuhumiwa na marehemu walikuwa na uhusiano wa kimapenzi hapo awali, na waliachana mara baada ya marehemu kubaini kuwa mtuhumiwa alikuwa anajihusisha na vitendo vya kihalifu hususan ni wizi na ujangili,” imesema taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi.
Aidha, wananchi wametakiwa kuacha kujichukulia sheria mkononi hususan katika kushughulikia migogoro ya kimapenzi, kwani zipo taasisi zinazoshughulikia changamoto hizo.
