Amuua baba mkwe baada ya kuwaamulia ugomvi

0
2

Polisi katika eneo la Mukaa, Kaunti ya Makueni nchini Kenya wameanzisha uchunguzi kufuatia tukio la kusikitisha ambapo mwanaume wa makamo anadaiwa kumuua baba mkwe wake na kumjeruhi vibaya mke wake wa zamani katika eneo la Kiou, kijiji cha Wathini.

Kwa mujibu wa Naibu Kamishna wa Kaunti ya Mukaa, Buxton Mayabi, mtuhumiwa ambaye alikuwa ametengana na mkewe, alimfuatilia hadi nyumbani kwao akiwa amejihami kwa panga.

Inadaiwa baada ya kufika katika makazi yake, alimshambulia mkewe kwa kumkata sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha makubwa.

Baba wa mwanamke huyo alipojaribu kuingilia kati, mtuhumiwa alimgeukia na kumshambulia kwa panga kwa nguvu kubwa. Mzee huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Sultan Hamud ambapo alithibitishwa kufariki dunia alipowasili.

Mwanamke huyo anaendelea kupokea matibabu katika hospitali hiyo na hali yake inaelezwa kuwa ya kuridhisha.

DCC Mayabi amesema mtuhumiwa alitoroka baada ya tukio hilo, lakini baadaye alijisalimisha katika Kituo cha Polisi cha Sultan Hamud ambako anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi.