
Ofisi ya Msajili wa Hazina imerekodi ongezeko la asilimia 40 katika makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi ndani ya kipindi cha miezi 11, ikilinganishwa na kipindi kama hicho katika mwaka wa fedha uliopita.
Akizungumza katika kikao na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo Juni 2, 2025, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema serikali imekusanya Sh884.7 bilioni kuanzia Julai 2024 hadi Mei 2025.
Hili ni ongezeko kubwa la mapato yanayokusanywa kutoka taasisi za umma na kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache, ikilinganishwa na Sh633.3 bilioni zilizokusanywa katika kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2023/24.
Pia hii inaonyesha ongezeko la asilimia 15.3 ikilinganishwa na jumla ya makusanyo ya mwaka mzima ya Sh767 bilioni katika mwaka wa fedha uliopita.
Bw. Mchechu alisema ukuaji huo wa mapato umetokana na kuimarishwa kwa utaratibu wa ufuatiliaji wa karibu wa gawio na michango katika Mashirika ya umma na matumizi ya Mifumo ya TEHAMA.
“Ofisi imefanikiwa kuunganisha Mfumo wa Mpango na Bajeti (PlanRep) na Mifumo ya ERMS na e-Watumishi pamoja na kufanya maboresho ya Mfumo wa MUSE ambao unawezesha kupata taarifa halisi za matumizi katika Taasisi na Mashirika ya Umma ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za Umma,” alisema Bw. Mchechu
Alisema maboresho hayo sasa yamefanya mifumo kubadilishana taarifa ipasavyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan aliyetaka kuona mifumo inasomana.
Akivitaja vyanzo vikuu vya mapato kwa mwaka huu amesema ni gawio ambalo limechangia asilimia 63.9 ya mapato yote, huku michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi ikichangia asilimia 29.7.
Aidha, mapato mengineyo yaliyojumuisha ziada, marejesho ya mikopo na riba pamoja na Mawasilisho yatokanayo na mtambo wa kuhakiki na kuwezesha mawasiliano (TTMS) yamechangia asilimia 6.4 ya mapato yote.
