Serikali na Sekta binafsi kuanzisha vituo vya kukodisha mitambo ya uchimbaji madini

0
6

Serikali kwa ushirikiano na sekta binafsi imejipanga kuanzisha vituo vya ukodishaji mitambo ya uchimbaji madini kwa wachimbaji wadogo ili kuwawezesha kutumia teknolojia za kisasa kufanya shughuli zao kwa tija.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde (Mb) wakati akihitimisha Kongamano la Maonesho ya Madini mkoani Mara kwenye viwanja vya Mukendo vilivyopo Manispaa ya Musoma.

“Sote tunatambua kwamba wachimbaji wadogo hawana uwezo wa kununua na kuihudumia mitambo ya kisasa kwa ajili ya uchimbaji.

Rais Samia Suluhu Hassan ametuelekeza Wizara ya Madini kuja na mpango huu ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata fursa ya kutumia teknolojia ya kisasa kwenye shughuli zao lengo la kuongeza tija na uzalishaji wa madini.

Sambamba na Mitambo ya kukodisha tunatarajia pia kuanzisha Kituo cha Elimu ya Uchenjuaji wa madini ambacho kitakuwa na Mtambo wa Uchenjuaji wa madini eneo la Nyamongo-Tarime.

Ni matarajio yetu sasa kwamba mpango huu unakwenda kubadilisha uchumi wa wachimbaji wadogo kwa kuinua vipato vyao na hatimaye kuongeza mchango zaidi kwenye ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na sekta ya Madini” amesema.

Amesema katika kipindi cha miaka minne ya Rais, Mkoa wa Mara umezalisha dhahabu tani 58.90 zenye thamani ya Shilingi Trilioni 6.90 kwa wachimbaji wadogo, kati na wakubwa.