Ulega: Rais Samia ameelekeza madeni ya wakandarasi wa ndani yalipwe

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Wizara yake inatekeleza kikamilifu maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha makandarasi wa ndani wanalipwa fedha zao, akisema kufikia sasa zaidi ya Bilioni 90 zimeshalipwa kwa makandarasi hao wa ndani wanaotekeleza miradi ya ujenzi.
Waziri Ulega amebainisha hayo leo Jumapili Juni 08, 2025 Jijini Mwanza wakati wa Mjadala uliofanyika kwenye daraja la Kigongo-Busisi, akibainisha kuwa Rais Samia ameelekeza kuwa kipaumbele cha malipo kwenye Wizara hiyo kuwa kwa makandarasi wazawa wanaoidai serikali.
“Katika muda mfupi ambao nimeanza kazi, jumla ya fedha zaidi ya bilioni 80 tumezilipa kwa makandarasi wa ndani. Kwahiyo deni la wakandarasi wa ndani lilikuwa zaidi ya bilioni 200 na zimebaki bilioni 180+. Tunaendelea kuwalipa hatua kwa hatua,” amesema.
Ameongeza kuwa “Ukweli ni kwamba kazi ya kuwalipa inaendelea hatua kwa hatua na kwenye jambo hili ukweli ni kwamba tunaendelea kuongeza kasi na nimewaeleza wataalamu wangu pale Wizarani kwamba hata fedha ikija kidogo kipaumbele cha kwanza kiwe ni kuwalipa wakandarasi wa ndani kwa sababu uchumi unazunguka humu ndani, tutawalipa na yote yatakwisha.”
