
Watu wengi huamini kuwa mafanikio au furaha hutokana na vitu vikubwa, kama utajiri, umaarufu au kuwa na bahati. Lakini kuna mambo madogo na ya msingi ambayo yanaweza kubadili kabisa namna tunavyoishi na kuona dunia.
Haya ni mambo matano yanayoweza kubadili maisha yako;
1. Maisha ni mchezo wa kuteseka, chagua ni matatizo gani uko tayari kuyakabili
Hakuna maisha yasiyo na matatizo. Tajiri ana matatizo ya pesa, masikini pia. Msanii ana changamoto zake, mfanyabiashara vilevile. Tofauti kubwa ni kwamba baadhi ya watu huchagua matatizo wanayotaka kuyashughulikia kwa sababu yanahusiana na kile wanachokipenda au kukithamini.
Mfano: Mtu anayependa kuimba, anaweza kuvumilia tabu za kushindwa au kukosolewa kwa sababu anapenda sana muziki. Badala ya kulalamikia kila tatizo, jiulize: “Je, hili tatizo ni sehemu ya maisha ninayotaka?” Ukichagua matatizo sahihi ya kukabiliana nayo, utayaona kama changamoto na sio mateso.
2. Badilisha maswali unayojiuliza
Mara nyingi tunashindwa kupata majibu sahihi kwa sababu tunajiuliza maswali mabaya. Maswali yako ni msingi wa fikra zako. Ukijiuliza, “Kwa nini mimi nashindwa?” utatafuta majibu mabaya. Lakini ukijiuliza, “Nawezaje kuimarika leo kuliko jana?” unajipa nafasi ya kukua.
Badilisha maswali unayojiuliza na utaanza kuona dunia kwa mtazamo mpya. Swali zuri hutoa mwelekeo chanya na suluhisho la kweli.
3. Jaribu na kisha ujifunze
Hatutakuwa na majibu yote kabla ya kuanza jambo. Usisubiri uhakika. Badala yake, chukua hatua ndogo, angalia matokeo, jifunze, kisha endelea. Kwa kufanya hivyo, utaelewa mambo kwa vitendo zaidi kuliko kufikiri tu.
Anza kwa kidogo. Jifunze kutokana na makosa. Kila hatua utakayochukua, hata kama ni ndogo, inakujenga kuelekea mafanikio. Hakuna aliyefanikiwa kwa kupanga pekee bila kuchukua hatua.
4. Tatizo si kwamba hujui cha kufanya, ni kwamba unaogopa
Karibu kila mtu anajua kinachotakiwa ili maisha yake yabadilike kama kula vizuri, kuacha uhusiano mbaya, au kufanya kazi kwa bidii. Lakini wengi wetu hatufanyi hivyo kwa sababu tunaogopa mabadiliko, maumivu au hukumu ya watu.
Hofu ni kawaida, lakini isiwe kikwazo. Chukua hatua hata kama unaogopa. Mabadiliko huja kwa ujasiri wa hatua, si kwa kukaa na kutafakari tu.
5. Kubali makosa yako hapo ndipo ukuaji huanzia
Hakuna aliyekamilika. Kila mtu hufanya makosa. Lakini watu wachache wana uwezo wa kusema, “Nilikuwa na makosa.” Kukubali kosa ni hatua ya kwanza ya kujifunza na kukua.
Ukweli ni huu: Watu wanaokubali makosa yao hujifunza haraka, huaminika zaidi, na huwa na uwezo mkubwa wa kubadilika kimaisha. Kukataa makosa ni kujifunga na kutojiruhusu kukua.