
Tume ya Ulaya imetangaza sasisho jipya la orodha ya nchi za tatu (zilizo nje ya Umoja wa Ulaya) zinazochukuliwa kuwa na hatari kubwa kutokana na mapungufu ya kimkakati katika mifumo yao ya kupambana na utakatishaji wa fedha na ufadhili wa ugaidi (AML/CFT).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, taasisi zote za kifedha ndani ya Umoja wa Ulaya (EU) zinazowajibika chini ya sheria za AML/CFT zinapaswa kuchukua hatua za tahadhari zaidi katika kushughulikia miamala inayohusiana na nchi hizo, ili kulinda mfumo wa kifedha wa EU dhidi ya uhalifu wa kifedha wa kimataifa.
Tume ya Ulaya imesema kuwa uamuzi huo umetokana na tathmini ya kina na ya kiufundi iliyofanyika kwa kuzingatia vigezo vya wazi pamoja na taarifa zilizokusanywa kutoka kwa Kikosi Kazi cha Kimataifa cha Kuzuia Utakatishaji Fedha (FATF), mazungumzo ya pande mbili na ziara katika nchi husika.
Hii ni orodha ya nchi zenye hatari kubwa ya utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi kwa mujibu ya Tume ya Ulaya;
- Algeria,
- Angola,
- Côte d’Ivoire,
- Kenya,
- Laos,
- Lebanon,
- Monaco,
- Namibia,
- Nepal
- Venezuela.
Wakati huohuo, baadhi ya nchi zimeondolewa kwenye orodha hiyo, ambazo ni: Barbados, Gibraltar, Jamaica, Panama, Ufilipino, Senegal, Uganda, na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).