Mbinu 6 za kifedha kwa wanandoa wapya

0
3

Kama ambavyo amani ni muhimu kwenye ndoa, fedha nayo ni sawa na oksijeni kwani huchangia kwa kiasi kikubwa kuleta amani kwenye maisha ya ndoa.

Wakati malaika wa ndoa akiendelea kuzifungulia ndoa kwa mwaka huu, hizi ni baadhi ya mbinu zinazoweza kuwasaidia wanandoa wapya kuepukana na changamoto kubwa za kifedha;

  • Weka kadi zako mezani

Hapa wanandoa wanapaswa kukaa chini na kuzungumza kuhusu pesa; mahusiano yao na pesa, matumizi yao ya muhimu ya kifedha kila mwezi, ikiwa wana madeni, vyanzo vyao vya pesa, na wategemezi wao hadi hapo walipo. Hiyo itawasaidia kujua mapato na matumizi yao kwa pamoja.

  • Tengeneza akaunti ya fedha ya pamoja

Kwa kuwa kila mmoja atakuwa na vitu vyake binafsi vya kufanya na pesa yake, ni vyema kuwa na akaunti nyingine ya pesa kwa ajili ya matumizi ya pamoja kama wanandoa. Ikiwa ni kwa ajili ya akiba na matumizi yenu ya kifamilia. Akaunti hii itatumika kuweka kiasi fulani cha pesa kila mwezi kutoka kwenye mapato yenu.

  • Tengeneza bajeti ya familia

Kutokana na kiwango mlichoweka pembeni na matumizi mliyoyataja, hapa mtachanganua ni matumizi gani yatatimizwa na pesa ya pamoja na yapi kwa pesa binafsi na kwa kipindi gani, ikiwemo matumizi ya nyumbani, burudani za pamoja na bili za kila mwezi.

  • Kuwa wakweli kuhusu hali zenu za kiuchumi

Unapoona kuna mahali unakwama ama unataka kuchukua mkopo, ni vyema kuzungumza na mwezio ili kujua mfanye nini kwa pamoja kuliko kuchukua mkopo kisha ukatoa taarifa baadaye pindi mambo yatakapokuwa magumu katika ulipaji. Wekeni utaratibu wa kuzungumzia hali zenu za kiuchumi hasa pale hali inapobadilika kwa kauli nzuri inayomfanya mwenzi wako asijisikie vibaya hata kwa makosa ya kiuchumi aliyofanya.

  • Anzisha mfuko wa dharura

Kila mwezi katika bajeti yenu hakikisha mnatenga kiasi cha fedha kama mfuko wa fedha za dharura endapo chochote kitatokea wakati wowote muwe tayari. Akaunti zote hizi mnazofungua ni vyema zikaandikwa majina yenu wote wawili. Mnaweza kuweka pesa kwa pamoja kila mwezi au kupokezana kuweka pesa kwenye akaunti hiyo.

  • Wekeni mipango ya kustaafu na matarajio yenu kiuchumi

Baada ya miaka mingi ya kazi, ni vyema kupanga namna gani mnapenda kustaafu na hali yenu ya kiuchumi, wapi mtaishi, na vyanzo vyenu vya kiuchumi  wakati huo ukifika.