
Maafisa wa Upelelezi kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) wamemkamata mwanamke mmoja kwa tuhuma za kumtapeli raia wa China kiasi cha shilingi za Kenya milioni 13 [TZS milioni 267.2] .
Mwanamke huyo, anayefahamika kama Harriet Mary Wabwire, mwenye umri wa miaka 38, anadaiwa kujitambulisha kama Mkurugenzi wa kampuni ya OTD Group Limited, na kumshawishi mfanyabiashara huyo wa China kuwa alikuwa na uwezo wa kumtumia vifaa vya aluminium alloys.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na DCI, Wabwire anadaiwa kughushi nyaraka ikiwemo stakabadhi ya usafirishaji (bill of lading) na cheti cha ubora kutoka Shirika la Viwango Kenya (KEBS), zilizoonesha kuwa mzigo wa kilo 23,890 za aluminium alloys ulikuwa umefungwa salama kwenye kontena la futi 40 tayari kusafirishwa kutoka bandari ya Mombasa kuelekea Ningbo, China.
Baada ya kupata imani ya mfanyabiashara huyo, Wabwire alipokea kiasi cha shilingi milioni 267.2 kupitia akaunti yake ya benki. Hata hivyo, mara baada ya fedha kuhamishwa, alizima simu yake na kutoweka.
Raia huyo wa China aliripoti tukio hilo kwa maafisa wa DCI, ambao walifanikiwa kufuatilia na kumtia mbaroni Wabwire akiwa mafichoni katika eneo la Tassia, Nairobi.
Kwa sasa mshukiwa anashikiliwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani hivi karibuni kujibu mashtaka ya utapeli, kughushi nyaraka, na kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu.








