Vyombo vya Habari vyalaumiwa kwa kuchochea maandamano Kenya

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Kipchumba Murkomen amevishutumu baadhi ya vyombo vya habari nchini humo kwa kuchochea vurugu wakati wa maandamano yaliyoongozwa na Gen Z siku ya Jumatano, akidai kwamba vilihusika moja kwa moja katika kuhamasisha waandamanaji kwa kisingizio cha kurusha matangazo mubashara.
Akizungumza siku moja baada ya Wakenya kuingia mitaani kuandamana, Murkomen ametetea uamuzi wa serikali wa kusitisha matangazo ya moja kwa moja wakati wa maandamano hayo, akisema ilikuwa hatua ya tahadhari kwa ajili ya kulinda usalama wa taifa.
Murkomen, amesema hakuna ubaya katika matangazo ya moja kwa moja kwa kuwa Kenya ina uhuru wa vyombo vya habari, lakini tatizo ni pale ambapo vyombo hivyo vinageuka kuwa kitovu cha uhamasishaji wa waandamanaji.
“Kwa kweli, vituo vingi vya habari vilionekana vikihamasisha watu kwa kusema… ‘ndiyo hawa tayari wamefika.’ Wanawahoji watu mitaani wakisema, ‘unawaambia nini wale ambao bado wako nyumbani?’ Hii ni kushiriki moja kwa moja katika kuhamasisha watu kuja mitaani,” amesema.
Zaidi ya hayo, Murkomen amedai kuwa baadhi ya vituo vya habari vilikuwa vikitoa maelekezo kwa waandamanaji kuhusu njia zinazofika kwenye maeneo nyeti ya serikali kama vile Ikulu.








