Ruto: Nitajenga kanisa Ikulu kwa pesa zangu mwenyewe

Rais wa Kenya, William Ruto amesema ujenzi wa kanisa katika Ikulu ya Nairobi hautagharimu pesa za walipa kodi isipokuwa pesa zake mwenyewe.
Akizungumza katika Ibada iliyoandaliwa na Dayosisi ya Kanisa la Anglikana la Kenya (ACK), Rais Ruto amesema ujenzi huo ni mpango unaolenga kuhudumia mahitaji ya kiroho ya wafanyakazi wa Ikulu na familia zao.
“Niwazi niseme, nitajenga hilo kanisa kwa pesa zangu mwenyewe. Gharama yake ni ndogo sana. Watu waache kupotosha umma kwa takwimu za uongo, propaganda hiyo hainitishi,” amesema Ruto.
Katika maelezo yake, Ruto ameonekana kumjibu moja kwa moja Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Kenya, Jackson Ole Sapit, ambaye hivi karibuni alihoji ikiwa Rais anataka kuwa askofu kwa kujenga kanisa katika Ikulu.
“Nimesikia mtu akiuliza kama sasa nataka kuwa askofu, la hasha! mimi ni muumini. Nitajenga hilo kanisa kwa ajili ya wafanyakazi zaidi ya 300 na familia zao walioko Ikulu, kwa kuwa wanastahili kuwa na mahali pazuri pa kuabudu, si kwa ajili ya sifa wala siasa,” amesisitiza.








