Maandamano Sabasaba: Mtoto apigwa risasi na kuuawa wakati akitazama televisheni

0
162

Maombolezo yametanda katika kijiji cha Ndumberi, Kaunti ya Kiambu nchini Kenya baada ya msichana wa miaka 12, Bridgit Njoki kupoteza maisha kwa kupigwa risasi ya bahati mbaya akiwa nyumbani akitazama televisheni.

Tukio hilo limetokea wakati wa maandamano ya Sabasaba yaliyofanyika nchini Kenya siku ya Jumatatu.

Kwa mujibu wa mama yake, Lucy Ngugi, tukio hilo lilitokea majira ya saa 12:20 jioni wakati familia ilikuwa nyumbani. “Tulikuwa nyumbani wote kama familia, ghafla risasi ilipenya ndani ya nyumba na kumpiga binti yangu kichwani,” alieleza kwa huzuni, akiongeza kuwa nyumba yao ipo umbali wa kilomita mbili kutoka barabara kuu ambapo maandamano yalikuwa yakiendelea.

Bridgit alikimbizwa katika Hospitali ya St. Brigid kwa matibabu ya dharura, lakini alifariki dunia akiwa katika juhudi za kuokolewa.

Tukio hilo limeibua hasira kutoka kwa wananchi na familia, wakitaka haki itendeke huku wakituhumu polisi kwa matumizi ya nguvu kupita kiasi ikiwemo risasi za moto dhidi ya raia wasiokuwa na silaha.

Send this to a friend