
Rais wa Kenya, William Ruto, ameagiza polisi kuwapiga risasi papo hapo wahalifu wanaojificha kama waandamanaji huku wakiteketeza na kupora mali za watu na biashara.
Akizungumza katika eneo la Kilimani alipokuwa akikagua mradi wa ujenzi wa makazi ya polisi unaoendelea, Rais Ruto amesema polisi wanapaswa kuwapiga risasi miguuni tu, ili waweze kupelekwa hospitalini na baadaye kufunguliwa mashtaka kwa uhalifu wao.
“Tunataka amani Kenya, watu wafanye biashara. Mtu ambaye anaenda kuchoma biashara na mali ya mtu mwingine, mtu kama huyo apigwe risasi miguuni, akienda hospitali, akienda kortini. Wasimuuwe lakini wapige miguu ivunjike. Hatuwezi kubali mtu anaenda kuchoma mali na biashara ya mwingine. Kuna haki hapo kweli? Askari wasipige wananchi risasi kuwaua lakini mhalifu ashughulikiwe,” amesema.
Rais Ruto amesisitiza kuwa wananchi wanahitaji mazingira ya utulivu ili kuendelea na shughuli zao za kila siku, hasa za kiuchumi, akionya vikali kuhusu uvamizi, uporaji na uchomaji wa mali, na kueleza kuwa hakuna atakayesamehewa katika msako dhidi ya wahusika.








