ACT yalalamikia Polisi kudai majina ya wagombea, Polisi wakanusha

Chama cha ACT Wazalendo kimelalamikia kile kilichoelezwa kuwa ni hatua ya Jeshi la Polisi na baadhi ya Wakuu wa Wilaya kuanza kuwasiliana na viongozi wa chama hicho wakitaka majina ya wagombea wa ubunge na udiwani, hatua iliyoitajwa kuwa batili na ya kuvuruga mchakato wa uchaguzi.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu amesema maeneo ya Kilwa, Kigamboni, Kinondoni, Magu na Tarime yameripoti mawasiliano hayo, ambayo ni kinyume na sheria, kwani majina ya wagombea huwasilishwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
ACT Wazalendo imesema tayari imewasilisha malalamiko kwa IGP, Msajili wa Vyama vya Siasa na INEC, na kuwaelekeza viongozi wake kutotoa taarifa yoyote kwa Polisi kuhusu wagombea.
Aidha, Jeshi la Polisi limesema barua hiyo haijamfikia Mkuu wa Jeshi la Polisi, na endapo itamfikia maudhui yake yatafanyiwa kazi kwa haraka ili kupata ukweli wake “ na mawasiliano hayo yametoka wapi na yametolewa na nani.”








