Akamatwa kwa kuwashawishi kingono na kuwatishia watawa wa Kibudha

0
116

Polisi nchini Thailand wamemkamata mwanamke aitwaye Wilawan Emsawat kwa tuhuma za kuwahadaa watawa wa dini ya Kibudha ili kuingia nao katika uhusiano wa kimapenzi na kisha kuwatishia watoe fedha nyingi ili kuficha mahusiano hayo.

Wilawan, mwenye umri wa kati ya miaka 30, alikamatwa nyumbani kwake katika jimbo la Nonthaburi, kaskazini mwa mji mkuu wa Bangkok, akikabiliwa na mashtaka ya ulaghai, utakatishaji fedha, na kupokea mali za wizi.

Taarifa za polisi zinaeleza kuwa Wilawan alilenga makusudi kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na viongozi wa juu wa dini ili kujinufaisha kifedha. Uchunguzi umebaini kuwa watawa kadhaa walihamisha kiasi kikubwa cha fedha baada ya kuingia katika mahusiano naye.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Uchunguzi, hadi sasa, takriban machifu tisa wa vituo vya watawa na watawa waandamizi wamelazimika kuvuliwa utawa kutokana na kashfa hiyo.

Ripoti ya polisi imeeleza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, akaunti za Wilawan zilipokea takriban baht milioni 385 [TZS bilioni 31.1], lakini sehemu kubwa ya fedha hizo ilitumika kwenye tovuti za kamari mtandaoni.

Uchunguzi ulianza baada mmoja wa kiongozi wa hekalu maarufu jijini Bangkok kujiuzulu ghafla. Ilibainika kuwa Wilawan alimweleza kuwa ni mjamzito na kumtaka ampe baht milioni 7.2 [TZS milioni 582.7] kama msaada wa kifedha.

Send this to a friend