
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imewapiga marufuku watangazaji wanne wa kituo cha redio cha Mjini FM kujihusisha na masuala ya kihabari kwa kosa la kufanya kazi bila kusajiliwa na kukiuka maadili ya taaluma ya habari.
Bodi imesema watangazaji hao ambao ni Deodatha William, Mussa Crispin Mgenge, Perfect Crispin na Iddy Bakari Iddy walikiuka haki ya faragha wakati wa mahojiano na msanii wa singeli, Dogo Paten, kutweza haki ya mhojiwa, kumlazimisha kutoa taarifa bila ridhaa yake na kumshushia hadhi yake.
“Kutokana na ukiukwaji huo mkubwa wa sheria na maadili ya taaluma ya habari, Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imewapiga marufuku watangazaji tajwa hapo juu kujihusisha na masuala ya kihabari kuanzia tarehe 18 Julai, 2025 mpaka hapo watakapotimiza matakwa ya sheria ikiwa ni pamoja na kuwa na sifa za kielimu na kuzingatia maadili ya taaluma ya habari,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, imesema watangazaji hao hawajasajiliwa na kupewa Ithibati na Bodi, hivyo wanafanya kazi za kihabari kinyume na kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 (Toleo la 2023).








