
Watu wawili wamefariki na wengine wawili kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha bajaji na gari lenye namba za usajili T 5677 DFA aina ya ZHONG THONG mali ya kampuni ya FRESTER iliyotokea eneo la Ibadakuli, Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga majira ya saa 5.00 asubuhi.
Jeshi la Polisi limesema miongoni mwa waliofariki ni aliyekuwa diwani wa Kata ya Solwa, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Awadh Hafiz (53) pamoja na Catherine Kazimili (39) mkazi wa Busanda Halmashauri ya Shinyanga.
Gari hilo lilikuwa likitokea Kahama kuelekea Mwanza likiendeshwa na Wahabi Abdallah (60) ambaye aligonga bajaji iliyokuwa ikiendeshwa na Issah Nicodem (52) na kusababisha vifo vya watu hao wawili.
“Majeruhi wa ajali hiyo ni Issah Nicodem, dereva wa bajaji na abiria wake Elias Wilson (18), mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari ya ufundi Mwadui, wanaendelea na matibabu katika hospitali ya Manispaa ya Shinyanga na hali zao zinaendelea vizuri,” imesema taarifa.
Jeshi la Polisi limesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi aliyeshindwa kuendesha gari hilo kwa tahadhari na kufuata sheria za usalama barabaran,i baada ya kujaribu kulipita gari lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara, na kugonga bajaji na kusababisha madhara.







