
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia dereva aitwaye Saimon Paul (29) mkazi wa Emaus Sanya Juu aliyekuwa akiendesha gari lenye namba za usajili T.822 CKA Toyota Hiace kwa kuligonga gari jingine kwa nyuma ambalo halijafahamika usajili wake na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi 11.
Ajali hiyo imetokea Julai 25, 2025 katika eneo la kwa Frank Kata ya Masama, Wilaya ya Hai majira ya saa moja na dakika 20 usiku.
“Uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo akiwa amelewa na kusababisha kupoteza umakini barabarani na matokeo yake kuligonga gari hilo ambalo halijafahamika kwa nyuma,” imesema taarifa ya polisi.
Aidha, majeruhi 10 wa ajali hiyo wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi na majeruhi mmoja anatibiwa Hospitali ya Wilaya ya Hai.








