Taharuki angani: abiria adai amebeba bomu ndani ya ndege

0
140

Abiria wa ndege ya shirika la easyJet waliokuwa wakisafiri kutoka Luton, Uingereza kwenda Glasgow, wamejikuta katika hali ya taharuki baada ya mwanaume mmoja kusimama katikati ya safari na kudai kuwa alikuwa na bomu ndani ya ndege hiyo.

Tukio hilo limeibua hofu kubwa miongoni mwa abiria, baada ya mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 41 kupaza sauti kwa kusema, “Simamisha ndege. Tafuteni bomu ndani ya ndege. Kifo kwa Marekani. Kifo kwa Trump.” Pia alisikika akirudia maneno ya Kiarabu ‘Allahu Akbar’ yenye maana ya Mungu ni mkuu.

Video ya tukio hilo, ambayo kwa sasa inachunguzwa na maafisa wa kupambana na ugaidi, inaonesha jinsi abiria walivyomdhibiti kwa haraka mwanaume huyo, ambapo mmoja alimwangusha chini na mwingine akimzuia. Abiria wengine walimpekua kutafuta vitu vyovyote hatarishi huku wakimhoji kuhusu madai yake na iwapo alikuwa ametumia pombe au dawa za kulevya.

Mmoja wa abiria alisikika akimuuliza, “Kwa nini umesema unataka kulipua ndege hii?” huku mwanamke mmoja aliyekuwa karibu akilia kwa huzuni akizungumza kwa simu na mpendwa wake.

Ndege hiyo ilipotua katika Uwanja wa Ndege wa Glasgow, polisi walimkamata mwanaume huyo. Wakati akiondolewa, aliomba simu na mkoba wake, ombi ambalo lilizua hasira kwa abiria wenzake.

Polisi wamethibitisha kuwa mtuhumiwa huyo bado anashikiliwa rumande huku uchunguzi ukiendelea. Hakuna abiria aliyejeruhiwa katika tukio hilo.

Send this to a friend