
Wahudumu wanne wa ndege waliokuwa ndani ya ndege ya Alaska Airlines aina ya Boeing 737 MAX 9 ambayo ilipata tatizo la mlango wa dharura kufunguka ghafla angani mwezi Januari mwaka jana, wamefungua mashtaka dhidi ya kampuni ya Boeing kwa madai ya kujeruhiwa kimwili na kuathirika kiakili.
Kwa mujibu wa gazeti la Seattle Times, wahudumu hao wanadai fidia kwa madhara ya sasa na ya baadaye, ikiwemo maumivu ya mwili, msongo wa mawazo, hofu na gharama nyingine walizopata kutokana na tukio hilo. Wakili wao, Tracy Brammeier, amesema wahudumu hao walionyesha ujasiri mkubwa kwa kuwasaidia abiria huku wakihofia maisha yao.
Mashtaka hayo yaliyowasilishwa katika Mahakama Kuu ya Kaunti ya King, mjini Seattle inaituhumu Boeing kwa kutengeneza ndege isiyo salama pamoja na uzembe katika utengenezaji wake. Hata hivyo, Boeing haikutoa maoni kuhusu suala hilo.
Mwezi uliopita, Bodi ya Kitaifa ya Usalama wa Usafiri (NTSB) ilisema kuwa Boeing haikutoa mafunzo sahihi na usimamizi wa kutosha, jambo lililosababisha tatizo hilo. Pia, ilibainika kuwa kampuni hiyo ilikosa kuweka bolti nne muhimu kwenye mlango wa dharura wa ndege hiyo wakati wa utengenezaji.







