Mwana FA na AY washinda rufaa fidia dhidi ya Tigo

0
167

Mahakama ya Rufaa Tanzania imewapa ushindi wasanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya, Hamis Mwinjuma (Mwana FA) na Ambwene Yesaya (AY), katika rufaa ya muda mrefu dhidi ya kampuni ya mawasiliano ya Tigo (sasa ikifahamika kama Honora), kuhusu matumizi yasiyoidhinishwa ya kazi zao za muziki.

Katika hukumu iliyosomwa leo, majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa wamebatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu uliokuwa umefuta fidia ya zaidi ya Shilingi bilioni 2.1 iliyokuwa imeamriwa na Mahakama ya Wilaya ya Ilala mwaka 2016, wakisema kuwa Mahakama ya Wilaya ilikuwa na mamlaka halali kusikiliza na kutoa uamuzi kuhusu shauri hilo.

Wasanii hao walifungua kesi hiyo wakidai kuwa nyimbo zao zilitumika na kampuni hiyo kama mialiko ya simu (caller tunes) bila makubaliano wala malipo yoyote.

Mahakama ya Ilala ilikubaliana na hoja zao na kuamuru walipwe fidia ya Shilingi bilioni 2.16 kama hasara maalum pamoja na Shilingi milioni 25 kama fidia ya jumla.

Hata hivyo, Tigo ilikata rufaa Mahakama Kuu, ambayo ilifuta hukumu hiyo kwa misingi ya kisheria ya mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo. Sasa, Mahakama ya Rufaa imeamua kuwa hoja hiyo haikuwa na msingi na kwamba Mahakama ya Wilaya ilikuwa na haki ya kusikiliza kesi hiyo.

Aidha, Mahakama ya Rufaa imeamuru kampuni ya Honora (Tigo) kulipa gharama zote za rufaa hiyo na kuagiza Mahakama Kuu kusikiliza rufaa nyingine 10 zilizowasilishwa na kampuni hiyo kuhusu masuala mengine ya msingi kwenye kesi hiyo.

Send this to a friend