
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameeleza kutoridhishwa na utekelezaji wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 400 kutoka Chalinze hadi Zuzu Dodoma ambao ulipaswa kuwa umefikia asilimia 31 lakini kwa sasa umefikia asilimia 24 tangu kuzinduliwa kwake Novemba, 2024.
Hali ya kusuasua kwa mradi imebainika wakati Dkt. Biteko akikagua mradi huo katika Kijiji cha Manchali wilayani Chamwino ambapo amemuagiza mkandarasi wa kampuni ya TBEA ya China kuhakikisha kuwa anafidia muda wa kazi uliopotezwa ili mradi ukamilike kwa wakati kutokana na umuhimu wake nchini.
Serikali ilikubaliana na mkandarasi kuwa mradi huo ufanyike ndani ya miezi 19 tu badala ya miezi 22 kwakuwa wakati mradi unazinduliwa tayari kazi kubwa za awali zilikuwa zimeshafanyika ikiwemo za upembuzi yakinifu na utoaji wa maeneo.
“Leo ni miezi saba imepita tangu tuzindue mradi sawa na asilimia 32 ya muda wote tuliokuwa tunahitaji kutekeleza mradi huu, na tulitegemea mradi kwa sasa ufikie asilimia 31 lakini katika hali ya kushangaza mradi umefikia asilimia 24 tu jambo ambalo halikubaliki,” amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko amesema sababu zilizotolewa na mkandarasi za kuchelewesha mradi ikiwemo ya wananchi kugoma kutoa maeneo kwa madai ya fidia hazikubaliki akieleza kuwa wananchi hao wana haki na lazima walipwe fidia, hivyo
ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutumia mapato yake ya ndani kulipa fidia wananchi waliopisha mradi.







