Ahukumiwa miaka saba jela kwa kuua bila kukusudia

0
97

Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro imemhukumu kifungo cha miaka saba jela Shigela Washa Buhimila (32), mkazi wa Tuliza Moyo, Wilaya ya Ulanga, baada ya kukiri kosa la kuua bila kukusudia wakati wa tukio la wizi wa mifugo.

Tukio hilo lilitokea usiku wa Desemba 23, 2024, eneo la Makingi, Kitongoji cha Popoto, Kijiji cha Mavimba, Kata ya Milola, Tarafa ya Lupiro, Wilaya ya Ulanga ambapo Shigela na mwenzake aliyefahamika kwa jina la Malege ambaye bado hajakamatwa, walimvamia na kumuua kwa kumkata sehemu mbalimbali za mwili Ntungwa Jiria Kitoga (50), mkazi wa kijiji hicho, wakati wakitekeleza wizi wa ng’ombe 22.


Ng’ombe hao walikutwa kwa mshtakiwa Shigela baada ya kukamatwa, na ushahidi dhidi yake uliweza kuthibitishwa mbele ya Mahakama.



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, amesema Jeshi la Polisi linaendelea na juhudi za kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu njia bora za kulinda mifugo yao, ikiwemo kushirikiana na vikundi vya ulinzi shirikishi.

Aidha, Jeshi la Polisi liameahidi kuendelea kuwasaka na kuwafikisha mahakamani wote wanaojihusisha na wizi wa mifugo.

Send this to a friend