TRA yakanusha mafuta ya kupikia kuingizwa kimagendo Bandari ya Bagamoyo

0
108

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mafuta ya kupikia kuingizwa nchini kupitia Bandari ya Bagamoyo bila kulipiwa kodi.

TRA imesema ni kweli mafuta ya kupikia yalihusishwa katika bandari hiyo na kulipiwa kodi zote stahiki kwa mujibu wa sheria na taratibu za forodha, pamoja na kukaguliwa kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari na taasisi za udhibiti wa viwango.

“Hivyo basi, haya mafuta ya kupikia hayakuingia kimagendo bali yamelipiwa kodi na yamepitia taratibu zote forodha,” imesema taarifa ya TRA.

Aidha, imesema utaratibu wa ushushwaji wa mafuta majini yamefanyika kwa sababu bandari rasmi ya Bagamoyo, Mbweni na Kunduchi, kwa sasa hazina gati. “Hata hivyo, Serikali inaendelea na maboresho makubwa ya Bandari ya Bagamoyo, yakiwemo ujenzi wa gati la kisasa la kushushia mizigo.”

TRA imesema itaendelea kushirikiana na vyombo vya dola kuchukua hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya magendo, ikiwemo kutaifisha bidhaa zote zinazohusika na magendo pamoja na kutoa adhabu kali.

Send this to a friend