
Mwanaume mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 45 na 50 amekutwa ameuawa kikatili kwa kukatwa mapanga mara kadhaa na watu wasiojulikana, mwili wake ukitelekezwa kando ya reli katika Mtaa wa Butunga, Kata ya Kibirizi, Kigoma.
Tukio hilo lilitokea Agosti 31, 2025, ambapo mwili wa marehemu uligunduliwa na wapita njia waliokuwa wakielekea kazini. Marehemu ametambuliwa kuwa ni fundi seremala mkazi wa Mtaa wa Gezaulole, Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, SACP Filemon Makungu, alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa mwili wa marehemu tayari umekabidhiwa kwa familia yake baada ya utambuzi kufanyika.
“Chanzo cha kifo bado hakijajulikana kwani mwili ulipatikana kando ya reli. Upelelezi bado unaendelea na utakapokamilika utatoa picha kamili ya alikotoka na kilichotokea,” alisema SACP Makungu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Butunga, Hamis Yasin, ametoa wito kwa vyombo vya usalama kuongeza jitihada za kuwasaka wahusika wa mauaji hayo.
Pia ameiomba polisi kuvunja makundi ya vijana wanaojihusisha na matumizi ya bangi na kamari haramu, akisema mara nyingi makundi hayo yana uhusiano na matukio ya kihalifu.







