Polisi yaanza uchunguzi mtoto mchanga kutupwa jalalani Geita

Jeshi la Polisi mkoani Geita limesema linafanya uchunguzi wa tukio la kifo cha mtoto mchanga, jinsia ya kiume, anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya Siku moja hadi mbili, aliyekutwa ametupwa kichakani huku mwili wake ukiwa umeungua moto.
Taarifa ya Polisi imesema tukio hilo limegundulika Septemba 01, 2025 majira ya asubuhi na kuripotiwa kituo cha Polisi. Mwili wa mtoto huyo umekutwa kichakani katika eneo la Mtaa wa Mwitulole, Kata ya Buhalahala, Manispaa ya Geita.
“Juhudi za kumsaka mtuhumiwa au wahalifu waliohusika katika tukio hili la kikatili zinaendelea ili waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria. Mwili umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Manispaa ya Geita kwa ajili ya uchunguzi, ” imesema taarifa hiyo.
Aidha, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kutoa taarifa za kihalifu mapema pindi wanapobaini matukio ya ukatili, ili hatua za kisheria zichukuliwe.








