Watano wakamatwa kwa tuhuma za utekaji Kenya

0
123

Maafisa wa upelelezi (DCI) katika Kaunti ya Kiambu wamewakamata watu watano wanaoshukiwa kuhusika na tukio la utekaji nyara huko Ruaka nchini Kenya.

Tukio hilo lilianza baada ya kijana mmoja kupotea ghafla. Rafiki yake wa kike alipompigia simu, ilijibiwa na mtu asiyejulikana ambaye alidai apewe shilingi 500,000 za Kenya [TZS milioni 9.5] ili kumuachilia. Binti huyo aliripoti kwa polisi, ambao walifanya msako wa haraka.

Kwa msaada wa taarifa za kiintelijensia, polisi walipata mahali walipokuwa watekaji katika eneo la Ithanga, na kumpata kijana huyo akiwa amejeruhiwa na akiwa na shati lenye damu.

Watuhumiwa waliokamatwa ni Sydney Ezra Achanda, John Louise Omondi, Enock Sum Cheruyot, Peter Kanini Mwangi, na Lucy Sara Muhonja.

Polisi pia wamekamata magari mawili yaliyotumiwa kwenye uhalifu huo aina ya Suzuki Swift nyekundu na Mazda Demio nyeupe. Ndani yake kukiwa na kisu, simu 10, na tablet.

Mamlaka zimethibitisha kuwa hadi wakati wa kukamatwa kwao, tayari watekaji walikuwa wamepokea shilingi 68,000 [TZS milioni 1.3] kama sehemu ya fidia waliyoitaka.

Send this to a friend