TRA yakanusha kutoza kodi kwa kila kitanda nyumba za wageni

0
116

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekanusha taarifa kuwa wamiliki wa nyumba za wageni wanatozwa kodi kwa kila kitanda. Badala yake, imeeleza kuwa kuna kodi ya uendelezaji utalii inayotozwa kwa baadhi ya hoteli na nyumba za wageni zilizotangazwa kwenye gazeti la Serikali, na kodi hiyo huhesabiwa kulingana na malipo ya malazi kwa siku, siyo kwa kitanda.

Meneja wa TRA Mkoa wa Kagera, Castro John, amesema tozo hiyo iliwekwa na Serikali kupitia kifungu cha 59(1) cha Sheria ya Utalii ya mwaka 2008 ili kusaidia kukuza na kuendeleza sekta ya utalii nchini. Tozo hiyo inahusu hoteli na nyumba za kulala wageni zilizosajiliwa na kutangazwa rasmi kupitia tangazo la Serikali (GN Na. 823 la tarehe 2/10/2020).

Amefafanua kuwa si tozo mpya, bali imekuwepo kwa muda kupitia kanuni zilizotangazwa kwenye gazeti la Serikali (GN Na. 352 la tarehe 1/10/2013), na inalipwa na wamiliki wa majengo yanayotoa huduma za malazi kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa masharti hayo, mmiliki wa nyumba ya wageni au hoteli iliyosajiliwa anatakiwa kulipa asilimia 1 ya gharama ya chumba iliyolipwa na mgeni, huku ritani na malipo ya kodi hiyo yakitakiwa kuwasilishwa kabla au ifikapo mwisho wa mwezi unaofuata.

Send this to a friend