Msigwa akanusha Uwanja wa Mkapa kufungwa kwa miezi 6

0
91

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Serikali haijatangaza kuufunga Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa miezi 6 kama ambavyo baadhi ya watu wanavyopotosha.

Katika taarifa yake, Msigwa amesema wamefanya makubaliano na klabu za Yanga na Simba ili kutafuta viwanja vingine kwa ajili ya michezo ya ligi, na Uwanja wa Benjamin Mkapa ubaki kwa ajili ya mechi za Kimataifa, Timu ya Taifa na Dabi mpaka hapo utakapofanyika ukarabati mkubwa wa eneo la kuchezea (pitch).

“Ni vizuri pia kujua kuwa uwanja mkubwa kama Benjamin Mkapa kila unapotumika ni lazima ufuatiwe na marekebisho kwa sababu hakuna tukio linaloweza kufanyika bila kusababisha uharibifu. Na hii sio kwa uwanja huu tu, ni viwanja vyote duniani, na ukarabati wake unahitaji utaalamu na sio kubondabonda,” ameeleza Msigwa.

Aidha, Msigwa amesema bilioni 13 zinazohojiwa na baadhi kutumika kukarabati uwanja huo hazikuhusisha ukarabati wa eneo la kuchezea badala yake zilifanya maboresho ya jengo, kuweka mifumo mipya ya umeme na taa, maji, vyoo, njia ya kukimbilia, kuweka viti vyote 62,000, kuweka viyoyozi, mfumo wa sauti, ubao wa matangazo, mabenchi ya ufundi, magoli, kupaka rangi na mfumo wa sauti.

Send this to a friend