Polisi wamsaka aliyemuua mwenzake kisa Simba na Yanga

0
83

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linamsaka Emmanuel Mabura (33), Bodaboda na mkazi wa Mtaa wa Mhandu Kisiwani, Wilaya ya Nyamagana kwa tuhuma za mauaji ya Mussa Said (34) ambaye anatuhumiwa kumchoma na kitu chenye ncha kali shingoni baada ya kuzuka ugomvi baina yao.

Taarifa ya Polisi imesema tukio hilo lilitokea Oktoba 19, 2025 majira ya saa 1 jioni ambapo mtuhumiwa alimchoma Mussa na kipande cha chupa baada ya kuzozana kuhusu mpira wa miguu uliohusisha timu ya Simba na Yanga, baada ya mtuhumiwa kuzidiwa hoja.

“Chanzo cha tukio hilo ni mzozo uliotokana na ushabiki wa mpira. Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kitaalamu na kukabidhiwa kwa ndugu kwa taratibu za mazishi,” imesema taarifa.

Aidha, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kufikishwa kwenye vyombo vya dola.

Send this to a friend