Mama atuhumiwa kuua watoto wake wawili kwa kuwazamisha mtoni

0
64

Mama mwenye umri wa miaka 24, Lillian Wacera Maina, amefikishwa mahakamani akikabiliwa na tuhuma za kuwaua watoto wake wawili kwa kuwazamisha katika Mto Mathioya, uliopo Kaunti ya Murang’a nchini Kenya.

Wacera anadaiwa kuwatupa binti zake, Precious Wanjiku (miaka 7) na Primrose Ngariuri (mwaka 1 na miezi 8), ndani ya mto huo siku tatu tu baada ya kuondoka nyumbani kwake Maralal, Kaunti ya Samburu.

Kwa mujibu wa taarifa za familia, mtuhumiwa alimdanganya mumewe kuwa alikuwa akisafiri kuelekea kijijini kwao Gatitu kumtembelea baba yake mgonjwa, kabla ya kutekeleza tukio hilo la kusikitisha.

Mahakama imeamuru Wacera aendelee kushikiliwa kwa siku 21 ili kuruhusu polisi kukamilisha uchunguzi, na kesi hiyo itatajwa tena Novemba 17, 2025.

Tukio hilo limeongeza idadi ya visa vya mauaji ya watoto vilivyoripotiwa katika Kaunti ya Murang’a. Hivi karibuni, mwanamke mmoja katika kijiji cha Kanorero, tarafa ya Kangema, alidaiwa kuwachoma kisu watoto wake wawili hadi kufa kufuatia ugomvi wa kifamilia, huku mtoto wa tatu mwenye umri wa miaka minne akinusurika baada ya kujeruhiwa kifuani.

Send this to a friend