
Serikali imetangaza mpango wa kuboresha miundombinu ya usafirishaji wa njia ya barabara unaojulikana kwa jina la Expressways Master wenye lengo la kurahisisha usafiri, kuongeza ufanisi na kukuza Pato la Taifa.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema mpango huo umeanza kutekelezwa na wataalamu wazalendo wa Tanzania kwa kushirikiana na wenzao kutoka Korea Kusini ambapo kwa sasa wataalamu wa pande zote wanakutana katika mafunzo maalumu ambayo yatatengeneza dira ya nini kitaenda kutokea kupitia mkakati huo.
“Lengo letu ni kwamba kupitia mafunzo haya, wataalamu wetu watapata ujuzi utakaowawezesha kujua namna ya kupanga, kutekeleza na kuendesha miradi mikubwa kabisa ya barabara,” amesema Ulega.
Waziri Ulega amesisitiza kuwa serikali imedhamiria kuboresha miundombinu yake usafirishaji ili iendane na wakati na mahitaji halisi ya wananchi.
Aidha, amewaasa wataalamu katika sekta ya ujenzi kuhakikisha wanapata ujuzi wa kubuni, kusimamia na kutekeleza ujenzi wa miradi inayoendana na malengo ya Dira ya Taifa ya mwaka 2050.
Kwa mujibu wa malengo ya mkakati huo, serikali imepanga kuhakikisha kwamba shoroba zote tisa za barabara nchini zinaunganishwa kwa barabara pana zaidi, zenye mfumo wa kidijitali, zinazohimili changamoto za kimazingira na zitakazosaidia maeneo ya uzalishaji kuunganishwa na masoko na bandari.








