Dkt. Nchimbi asisitiza uhuru wa mahakama usitumike kuminya haki

0
32

Makamu wa Rais, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema uhuru wa mahakama usitumike kama sehemu ya kuficha uzembe, upendeleo au vitendo visivyo vya haki, amesema uhuru huo ni dhamana ya kutenda haki kwa uadilifu, uwazi na kwa kuzingatia katiba na sheria za nchi.

Amesema hayo, wakati alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria yaliyofanyika Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.

Balozi Dkt. Nchimbi amesema mahakama ina wajibu muhimu wa kulinda utawala wa sheria, kusimamia utekelezaji wa mikataba, kulinda rasilimali za taifa, na kuhakikisha kuwa maendeleo yanayopatikana yanawanufaisha Watanzania wote kwa usawa.

Aidha, amesema kwa kutambua umuhimu wa mahakama katika ujenzi wa taifa, serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi katika kuimarisha uhuru wa mahakama ili kuiwezesha kutekeleza wajibu wake kikamilifu.

Mbali na hayo, Makamu wa Rais amewaasa viongozi, wanasiasa, wanaharakati na wananchi mbalimbali kuheshimu tume iliyoundwa na Rais ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa kuacha kuongelea masuala hayo nje ya mfumo wa kisheria.

Send this to a friend