Siku 100 za Rais Samia: Serikali yaweka historia ujenzi wa miundombinu

0
24

Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha miradi 40 ya madaraja ya dharura kati ya 81, ikiwemo mradi wa King’ori, yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 500, unaotekelezwa chini ya programu maalumu ya Contingent Emergency Response Component (CERC). Miradi hiyo imelenga kutatua changamoto na kuleta tabasamu kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari na wananchi wa King’ori, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema mafanikio hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Siku 100 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani, zilizolenga kuimarisha ujenzi wa barabara na madaraja nchini.

Ulega ameongeza kuwa Serikali imetoa fedha hizo ndani ya siku 100 kwa ajili ya kulipa makandarasi waliotekeleza miradi ya ujenzi nchini, akibainisha kuwa Shilingi bilioni 280 zimetolewa na Hazina, huku kiasi kilichobaki kikitoka kwa wafadhili.

Aidha, amesema katika eneo la King’ori, Serikali imefanikiwa kujenga madaraja sita makubwa ya kupitisha maji kutoka milimani, kuweka taa 136 za barabarani, kujenga kilometa moja ya barabara ya lami, pamoja na vituo viwili vya daladala. Ameeleza kuwa huduma hizo zimetekelezwa ili kuleta tabasamu na utu kwa wananchi wa eneo hilo.