
Sekta ya madini inaendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa Tanzania, ikichangia takribani asilimia kumi ya pato la Taifa na kuunganisha maelfu ya shughuli za kibiashara katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini. Ingawa migodi mikubwa mara nyingi hupata uangalizi zaidi, wakati shughuli nyingi za kila siku za sekta hii zinaendeshwa na wachimbaji wa kati, wasambazaji, wakandarasi, wasafirishaji na watoa huduma wengine wanaotegemea upatikanaji wa huduma za kifedha kwa uhakika ili kuendesha shughuli zao.
Benki ya Stanbic Tanzania imesema kuwa kupitia kitengo chake cha Biashara kwa Wateja wa Kati, imejikita kuimarisha uwezeshaji kwa biashara hizi kwa kutoa suluhisho za kifedha zinazoendana na hali halisi ya shughuli zao, kusapoti mwendelezo wa biashara, kudhibiti Athari za uhatarishi na kuwezesha ukuaji endelevu katika mfumo mzima wa sekta ya madini.
Sekta ya madini ni chanzo cha pili kwa ukubwa wa uingizaji wa fedha za kigeni nchini baada ya sekta ya utalii, huku madini ya dhahabu yakiongoza. Zaidi ya uchimbaji wenyewe, sekta hii inaunga mkono mtandao mpana wa biashara za ndani zinazofanya kazi katika maeneo ya migodini, zikiwemo kampuni za vifaa, usafirishaji, uhandisi na huduma mbalimbali, ambazo mchango wao unaathiri moja kwa moja tija na uimara wa mnyororo wa thamani wa madini.
Kupitia kitengo cha Biashara kwa Wateja wa Kati, Benki ya Stanbic Tanzania inatoa huduma za kifedha zilizobuniwa kwa kuzingatia uzoefu halisi wa wachimbaji wa kati na biashara zinazohusiana na madini. Ushirikiano wa karibu na wateja katika mikoa mbalimbali yenye madini umebaini changamoto mbali mbali zinazowakabili kama vile mizunguko isiyotabirika ya malipo, gharama kubwa za vitendea kazi, gharama za matengenezo ya mitambo, changamoto za ubadilishaji wa fedha za kigeni pamoja na gharama za nishati.

Elias Ngunangwa, Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja wa Mashirika na Uwekezaji na Mollen Charles, Meneja Uhusiano Mwandamizi chini ya Biashara za Kibenki wa Benki ya Stanbic Tanzania wakiwa kwenye mkutano wa Mining Indaba mjini Capetown, Afrika Kusini hivi karibuni.
Huduma za mikopo ya mtaji kazi husaidia biashara kuendesha shughuli za kila siku na kudhibiti mtiririko wa fedha. Aidha, mikopo ya ununuzi wa mitambo na vifaa husaidia kuongeza tija, usalama na ufanisi wa kazi, huku mikopo ya magari ikirahisisha shughuli za usafirishaji na usimamizi.
Benki pia inatoa huduma za bima kulinda mali, wafanyakazi na shughuli za biashara katika sekta yenye hatari za kiutendaji na kimazingira, pamoja na huduma za kudhibiti hatari za ubadilishaji wa fedha kwa biashara zinazohusika na uagizaji au usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi. Kadri umuhimu wa nishati unavyozidi kuongezeka, Benki ya Stanbic Tanzania inaunga mkono pia matumizi ya nishati mbadala ikiwemo nishati ya umeme jua ili kusaidia biashara za madini kupunguza gharama za uendeshaji.
Akizungumza kuhusu mtazamo wa benki mara baada ya kumalizika kwa mkutano mkubwa wa madini wa Mining Indaba uliomalizika mwishoni mwa wiki jijini Cape Town, Afrika Kusini, Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Biashara katika Benki ya Stanbic Tanzania, Mollen Charles, alisema lengo ni kuwezesha kwa vitendo inayoendana na changamoto halisi za biashara zinazohusiana na sekta ya madini.
“Lengo letu ni kuhakikisha wachimbaji wa kati na biashara zinazowaunganisha wanapata huduma sahihi za kifedha katika kila hatua ya safari yao. Kwa kuunganisha mikopo ya mtaji kazi, ununuzi wa mitambo, bima na suluhisho za nishati endelevu, tunawezesha biashara kuendelea kufanya kazi, kudhibiti uhatarishi na kukua kwa namna inavyonufaisha jamii za migodini na uchumi kwa ujumla,” alisema Charles.







