Serikali yakanusha upotoshaji kuhusu uchunguzi Saratani ya Matiti

0
9

Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala limekanusha taarifa inayosambaa mitandaoni kuwa uchunguzi wa Saratani ya Matiti kwa kutumia ‘biopsia’ husababisha saratani kuenea.

Baraza limefafanua kuwa, mtu anayeonekana kwenye video inayosambazwa si mtaalamu wa tiba asili na wala hatambuliki na baraza lolote la kitaaluma nchini, na kwamba baada ya ufuatiliaji limegundua mhusika anajihusisha na biashara za bidhaa za kimtandao (network marketing) na wala hatakiwi kuelimisha jamii masuala ya afya.

“Biopsia ni njia salama, ya msingi na inayotambulika duniani kote katika kuthibitisha aina ya saratani ili kusaidia kupanga matibabu sahihi kwa wakati. Madai kwamba biopsia husababisha saratani kusambaa ni upotoshaji unaoweza kuhatarisha maisha ya wagonjwa, ” imeeleza taarifa ya baraza hilo.

Aidha, Baraza limeelekeza wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala, wafanyabiashara na wajasiriamali wa bidhaa mbalimbali wanaotoa elimu au kutumia bidhaa hizo kwa madai ya kimatibabu kuondoa mara moja matangazo yote yanayopotosha jamii, kwani yanaweza kuchelewesha wagonjwa kupata matibabu sahihi na kuwanyima haki yao ya msingi ya huduma bora za afya.