Mshambuliaji kinda wa Serengeti Boys aitwa Taifa Stars
Kocha mkuu wa timu ya Taifa Tanzania, Emmanuel Amunike amemuita mshambuliaji wa Serengeti Boys, Kelvin John katika kikosi chake cha wachezaji 39, kinachojiandaa na fainali za Mataifa ya Afrika Misri.
Katika kikosi iko cha awali amewaita wachezaji kutoka klabu mbalimbali wakiwemo nyota wawili kutoka timu za vijana chini ya miaka 20 na 17, pia amewarejesha Abdi Banda na Ibrahim Ajib.
Amunike amewaita Kelvin John na Claryo Boniface kutoka katika timu ya taifa ya vijana U20 katika orodha hiyo ya nyota 39, pia ndiyo itakayotoa wachezaji watakaounda kikosi cha Tanzania kitakachocheza mechi ya awali ya kusaka kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).
Katika kusaka kufuzu kwa CHAN mwakani Tanzania itaanza kwa kucheza dhidi ya Sudan mwishoni mwa Julai.
Akitangaza majina hayo Amunike alisema ameita wachezaji chipukizi kwa lengo kubwa la kuwaweka katika misingi imara ya maendeleo ya baadaye.
“Kuna wachezaji watastaafu kwahiyo tumeita wachezaji vijana kwaajili ya baadae, pia kuna mashindano ya Afcon na baadaye Chan ndio maana nimeita wachezaji 39,” alisema.
Aliongeza anahakikisha wanapata mechi za kirafiki ngumu ili kuwa fiti kuelekea katika Afcon nchini Misri.
“Tunahitaji michezo mingi tuna mpango wa kucheza na Misri pia hata Nigeria, tutaona namna ambavyo itakavyokuwa, lakini hao ni miongoni tutakaocheza nao, lengo siyo matokeo lakini kucheza na timu iliyotuzidi ili kujua mapungufu na mazuri yetu,” alisema
Kikosi Taifa Stars:
Aish Manula (Simba), Metacha Mnata (Mbao), Claryo Boniface (undr20), Suleman Salula (Malindi fc), Aron Kalambo (Prison), Hassan Kessy (Nkana Fc), Vicent Philipo (Mbao), Shomari Kapombe (Simba), Gadiel Michael (Yanga), Abdi Banda (Baroka), Ally Mtoni (Lipuli), Mohammed Hussein (Simba).
Pia Agrey Morris (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Erasto Nyoni (Simba), David Mwantika (Azam), Ally Ally (Kmc), Kennedy Wilson (Singida) Feisal Salum (Yanga).
Himid Mao (Petrojet), Mudathir Yahya (Azam), Yahya Zaydi (Ismailia), Jonas Mkude (Simba), Ibahim Ajib (Yanga), Fred Tangaru (Lipuli Fc), Frank Domayo (Azam fc), Shaban Chilunda (Tenerife afc), Shiza Ramadhan (Enppi), Simon Msuva (al Jadida).
Wapo Rashid Mandawa (Bdf Xi), Mbwana Samatta (Krc Genk), Thomas Ulimwengu (JS Saoura), John Bocco (Simba), Farid Mussa (Teneriffe), Ayoub Lyanga (Coastal Union), Kassim Hamis ( Kagera Sugar), Miraj Athuman (lipuli), Kelvin John (undr 17) na Adi Yusuph (Solihull Moors, England).