Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amemsimamisha uanachama wa Bunge la Afrika, Stephen Masele ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika kutokana na makosa ya nidhamu.
Mbali na kumsimamisha, Spika pia amemuita nchini mbunge huyo kwa ajili ya mahojiano kutokana na utovu wa nidhamu alioufanya.
Spika Ndugai ameyasema hayo leo bungeni ambapo ameeleza kuwa Stephen Masele ametenda makosa ya kinidhamu na kwamba amemtumia wito wa kuja nchini ambapo atahojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka pamoja na Kamati ya Maadili ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Amesema kuwa kiongozi huyo wa chombo hicho cha Afrika amekuwa akitoa maneno ya uongo ambapo ni pamoja na kugonganisha mihimili ya dola kwa maneno hayo na kwamba ushahidi upo.
Licha ya kumtumia wito huo, Spika amesema kuwa Masele amekaidi kuja nchini, akidai kwamba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ndiye aliyemwambia apuuze wito huo.
Katika barua yake ya leo Mei 16, Spika wa Bunge ameeleza uamuzi huo wa kumsimamisha uanachama Masele, hadi pale Kamati ya Bunge ya Maadili itakapomalizana naye.
Hapa chini ni kauli ya Spika Ndugai kuhusu sakata hilo:
Masele ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, na pia amewakuwa Kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini (kabla wizara hiyo haijavunjwa na kuwa wizara mbili tofauti).