Abiria wanaoenda Mwanza wakwama stendi ya Magufuli kwa saa 10

0
64

Taharuki imezuka katika kituo kikuu cha mabasi cha Magufuli (Magufuli Terminal) mkoani Dar es Salaam baada ya basi la kampuni ya Kidia One Express ambalo lilitakiwa kusafiri alfajiri leo Desemba 23, 2022 kutoka jijini Dar es Salaam kuelekea Mwanza kutokuwasili kituoni hapo na kuwaacha abiria katika sintofahamu kubwa.

Akizungumza na Swahili Times mmoja wa abiria hao, Rehema Abdul amesema abiria walifika kituoni tangu alfajiri kwa ajili ya kuanza safari lakini ilipofika saa moja gari hilo lilikuwa bado halijafika kituoni, ndipo alipoamua kumpigia wakala wa kampuni hiyo ambaye alidai kuwa “gari liko service [linafanyiwa matengenezo] kwa kuwa lilifika usiku sana hivyo wawe wavumilivu hadi saa 1:30.”

“Ilipofika saa nne tuliwafuata LATRA maana wako hapa tukawaeleza wakasema gari ina matengenezo, tukamchagua mtu mmoja aende kituo cha polisi akazungumze nao, majibu yaliyokuja ni kwamba tusubiri gari mpaka saa tano itakuwa tayari, tumekaa mpaka saa tano hatuoni gari. Mpaka kufikia saa saba tukaenda tena ofisini wakasema mnataka majibu ya aina gani kama mnataka mkachukue pesa zenu,” ameeleza Rehema.

Amuua mkewe baada ya kuambiwa mtoto si wake

Aidha, abiria wamedai gari hilo limefika kituoni hapo saa 9 alasiri, huku wakilalamikia baadhi ya viti vya basi kukosa mikanda kwa ajili ya usalama.

Kwa upande wake Afisa Mfawidhi kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), Eyudi Nziku amethibitisha kuwa ni kweli gari lilikuwa likifanyiwa matengenezo, na kwamba walikuwa wakishirikiana na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha kuwa gari hilo ni salama kwaajili ya safari.

Hata hivyo, Swahili Times ilipozungumza na kampuni ya Kidia One asubuhi, walidai gari hilo lilikuwa ‘garage’ hivyo liko njiani kuelekea kituoni kuwachukua abiria, na hadi kufikia saa 10 jioni gari liliwasili kituoni kwa ajili ya safari ya kuelekea Mwanza ambayo huchukua zaidi ya saa 15.

Send this to a friend