ACT-Wazalendo yagoma Mpina kuondolewa kugombea Urais

0
127

ACT-Wazalendo imesema haitafuata maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo yamebatilisha uteuzi wa Luhaga Mpina kugombea Urais wa Tanzania kupitia chama hicho.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa chama, Ado Shaibu, imesema kwa hatua iliyofikiwa na msajili hana mamlaka ya kuingilia mchakato isipokuwa kwa njia ya pingamizi. Imesema Tume ya Uchaguzi tayari imeshatoa fomu na wagombea wanaendelea na taratibu za ujazaji  wa fomu.

“Msajili wa Vyama vya Siasa hana mamlaka ya kuingilia mchakato huo isipokuwa kwa njia ya pingamizi,” imesema taarifa hiyo.

Imeongeza kuwa “Mgombea wa Urais wa Tanzania, Luhaga Mpina amechukua fomu, amezijaza, amezunguka nchi nzima kusaka wadhamini, amekula kiapo mahakamani na kukamilisha taratibu. Leo fomu hizo zimehakikiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na kesho saa 7:00 mchana zitawasilishwa Ofisi ya Tume Huru ya Uchaguzi kwa ajili ya uteuzi.”

Aidha, Chama hicho kimesema kwamba kitafungua kesi Mahakama Kuu kupinga hatua hiyo na kuweka zuio dhidi ya utekelezwaji wa uamuzi huo.

Send this to a friend