ACT Wazalendo yazitaka nchi za Afrika kuungana na Afrika Kusini kupinga uamuzi wa Marekani
![](https://swahilitimes.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/act-pic-905x613.jpg)
Chama cha ACT Wazalendo kimeeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump, wa Februari 8, 2025, wa kukata misaada ya kigeni kwa Afrika Kusini. Hatua hiyo inakuja kama adhabu kwa msimamo wa Afrika Kusini katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ambapo imeishikilia Israel kuwajibika kwa mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina na pia kwa juhudi zake za mageuzi ya ardhi kurekebisha dhuluma za kihistoria.
Katika taarifa yake, ACT Wazalendo imeeleza kuwa hatua hii inaonesha dharau ya wazi ya Marekani kwa uhuru wa mataifa ya Afrika na haki za kimataifa. Chama hicho kimesema kuwa Marekani imeendelea kutumia misaada ya kigeni kama silaha ya kulazimisha mataifa mengine kutii matakwa yake, lakini hatua ya sasa ni hatari zaidi kwani ni shambulio la moja kwa moja dhidi ya haki ya Afrika Kusini kutekeleza mageuzi ya ardhi yanayolenga kurekebisha unyang’anyi wa ardhi uliofanywa wakati wa ukoloni.
Chama hicho kimeeleza kuwa upinzani wa Marekani dhidi ya Sheria ya Unyang’anyi wa Ardhi Na. 13 ya 2024, ambayo inalenga kuwapatia ardhi Waafrika Kusini waliotengwa kihistoria, ni ishara ya juhudi za Washington kulinda mifumo ya kiuchumi ya enzi za ubaguzi wa rangi kwa gharama ya haki.
Aidha, ACT Wazalendo imelaani vikali matumizi ya misaada kama zana ya shinikizo la kisiasa na kueleza kuwa uamuzi wa Marekani siyo tu shambulio dhidi ya Afrika Kusini, bali ni dharau kwa haki ya Afrika kujiamulia mustakabali wake bila kuingiliwa kutoka nje. Chama hicho kimesisitiza kuwa vitisho hivi lazima vikabiliwe kwa upinzani madhubuti.
ACT Wazalendo imezitaka nchi zote za mstari wa mbele barani Afrika kupinga unafiki wa Marekani kwa kuungana na Afrika Kusini, kutathmini upya uhusiano wao wa kidiplomasia na Marekani, na kutafuta ushirikiano unaojali usawa, heshima, na haki ya kujitawala.
“Tunathibitisha mshikamano wetu na Afrika Kusini katika jitihada zake za kupambana na mabaki ya mifumo ya ubaguzi wa rangi na kutafuta haki kwa watu wa Palestina,” inasomeka sehemu ya taarifa ya ACT Wazalendo. Chama hicho pia kimetambua na kupongeza msimamo thabiti wa Economic Freedom Fighters (EFF) na Chama cha African National Congress (ANC) dhidi ya shinikizo la Marekani linalolenga kuzima harakati za Afrika Kusini za haki na kujitawala.