
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamsaka Bagandosa Silas Menelo kwa tuhuma za mauaji ya Elias Martine Mshaki (23), mkazi wa kijiji cha Lumeya, wilayani Sengerema baada ya kumfumania akiwa na mke wake nyumbani kwake.
Tukio hilo lilitokea Julai 29, 2025 saa 1:00 asubuhi Kijiji cha Lumenya, kata ya Nyakaliro, wilayani humo ambapo mtuhumiwa anadaiwa kumuua Mshaki kwa kumpiga na kitu butu tumboni na kisha kumjeruhi mke wake, Neema Thobias (20) kwa kumpiga na kitu butu kwenye sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha kichwani.
“Inadaiwa kuwa mtuhumiwa Bagandosa na marehemu walikuwa wanakunywa pombe pamoja na baadaye marehemu alimnunulia mtuhumiwa pombe na kumuacha akiendelea kunywa na yeye kwenda nyumbani kwa mtuhumiwa mpaka alipokutwa na mtuhumiwa akiwa na mke wa mtuhumiwa,” imesema taarifa.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa na upelelezi unaendelea.








