Adaiwa kumuua mkewe kwa kumnyima tendo la ndoa

0
47

Jeshi la Polisi mkoani Njombe limesema chanzo cha mtuhumiwa wa mauaji, Juma Kyando kwa mke wake, Tumaini Luvanda (35) ni ugomvi wa kifamilia wa muda mrefu uliosababishwa na kunyimwa tendo la ndoa.

Mwanaume huyo anadaiwa kumuua mke wake kwa kumkatakata viungo vyake kisha kuvitia kwenye mfuko na kuvitupa kwenye mto ulio jirani na nyumba yake eneo la Kabinda mkoani humo.

Akisimulia tukio hilo, kamanda wa polisi mkoani humo, Mahamoud Banga amesema siku ya tukio marehemu alichelewa kurudi na alipoulizwa na mume wake hakutoa maelezo mazuri na ndipo mume huyo alipopandwa na hasira na kisha kutekeleza tukio hilo.

Majirani wameeleza wasiwasi wao kwa mtuhumiwa huyo wakidai pengine alipatwa na matatizo ya akili jambo ambalo polisi inafanya utafiti zaidi wa kitaalamu japokuwa ndugu zake wamedai ndugu yao hana historia yakuwa na magonjwa ya akili.

Akizungumza Diwani wa Iwawa, Francis Chaula amewaomba viongozi wa dini kuwa makini juu ya mikesha inayofanyika kwani inasababisha migogoro mingi ya kifamilia na kuvunja ndoa.

Chanzo: Mwananchi

Send this to a friend