Afariki baada ya kuanguka kwenye mnazi alioukwea akiwa amelewa

0
42

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kusini Unguja, Suleiman Hassan Suleiman amethibitisha kutokea kwa kifo cha Said Ali Said (44) Mkazi wa Miwani, wilaya ya Kati Kusini  anayedaiwa kuanguka kutoka juu ya mnazi akiwa amelewa.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda Suleiman amesema Machi 29 mwaka huu majira ya saa 1:00 asubuhi, kijana huyo alipanda mnazi akiwa amelewa chakari na mwishowe kuanguka na kupata maumivu makali ambayo yalisababisha kifo chake.

Aidha, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Hussein Ali ameeleza kwamba baada ya kupata taarifa ya kuanguka kwa Said walikwenda mara moja kwenye eneo la tukio na kumkimbiza katika Hospitali ya Mnazi mmoja kwa ajili ya matibabu.

“Baada ya kufika kwenye tukio niliwafuata vijana wenzangu tukashirikiana na kumpeleka hospitalini, lakini baada ya uangalizi wa daktari aligundua kuwa tayari amekwishafariki,” amesema Hussein.

Hata hivyo ACP Suleiman ametoa wito kwa watu wenye tabia za ulevi kuwa makini na kujiepusha na vitendo vitakavyohatarisha maisha yao.

Send this to a friend