Afisa Habari wa KenGold ahukumiwa kwa kuomba na kupokea rushwa

0
5

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu kulipa faini ya shilingi milioni 1 au kwenda jela miaka miwili Afisa Habari na Mawasiliano wa Klabu ya KenGold, Joseph Mkoko (34) baada ya kupatikana na hatia ya kuomba na kupokea rushwa.

Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki ametoa hukumu hiyo Juni 11, 2025 baada ya mshtakiwa huyo kukiri mashtaka hayo ya rushwa yaliyofanyika kati ya Desemba 01, 2024 hadi Desemba 31, 2024 Kibaha, mkoani Pwani.

Imeelezwa kuwa mshtakiwa aliomba rushwa ya shilingi milioni 1.5 toka kwa mchezaji wa zamani wa timu ya mpira wa miguu ya Vital’O ya Burundi, ili amsaidie kusajiliwa KenGold, na kupata upendeleo wa kupangwa kikosi cha kwanza ambapo ni kinyume na kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2024.

Mkoko amekiri mashtaka yake wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili kusomewa hoja za awali. Baada ya hukumu hiyo mshtakiwa amelipa faini na kukwepa kifungo.